Yesu alipopaa kwenda mbinguni aliwaachia wanafunzi wake angalizo juu ya siku ya kuabudu. Alisema, “Ombeni, ili kukimbia kwenu kusiwe wakati wa baridi, wala siku ya sabato.” (Mathayo 24:20). Alitambua kuwa kanisa lake lingepata usumbufu mkubwa wakati wa kuangamia kwa Yerusalemu kulikotokea mwaka wa 70 AD. Aliona hatari mbili juu ya tukio hilo. Kama lingetokea wakati wa baridi lingeongeza maafa maana uwezekano wa watu wengi kufa kwa ajili ya baridi ulikuwa dhahiri. Licha ya matatizo ya kiafya na kimwili aliona tukio hilo lingeleta usumbufu wa kiroho na hasa lilikuwa na uwezekano wa kutatiza ibada. Kwa kuwa siku hiyo ya ibada yaani siku ya saba ya juma haiwezi kuhamishika aliwaomba waumini wake kusali sana ili Mungu aepushe tukio hilo lisitokee siku ya Sabato. Alifanya hivyo kuwaonesha umuhimu wa siku hiyo hata baada ya kuondoka kwake.
Wanawake waliokwenda kuuangalia mwili wa Kristo kaburini, alipokufa siku ile ya Ijumaa, walikumbuka agizo la Yesu na siku inayofuatia ya Jumamosi walipumzika na kujielekeza kwenye ibada bila kujali kuwa walikuwa kwenye uchungu mkubwa wa kumpoteza Bwana wao. “Wakarudi, wakafanya tayari manukato na marhamu. Na siku ya sabato walistarehe kama ilivyoamriwa.” (Luka 23:56) Mitume walipokea wosia huo na kuitunza siku hiyo ya ibada katika vizazi vyao vyote. “Na Paulo, kama ilivyokuwa desturi yake, akaingia mle walimo, akahojiana nao kwa maneno ya maandiko sabato tatu.” (Matendo 17:2). Sabato iliendelea kutunzwa kwa karne kadhaa wakristo wakiwa hawajui siku nyingine ya kumuabudu Mungu isipokuwa siku ya saba ya juma yaani Jumamosi. “Hata siku ya sabato tukatoka nje ya lango, tukaenda kando ya mto, ambapo tukadhani ya kuwa pana mahali pa kusali; tukaketi, tukasema na wanawake waliokutana pale.” (Matendo 16:13)
Madai ya kuhamisha siku ya ibada kutoka siku ya saba ya juma yanapatikana katika vitabu vya kihistoria na wala si katika Maandiko Matakatifu. Usingetegemea kupata badiliko hilo kutoka vitabu vitakatifu kwa kuwa Mungu ameahidi kutobadilisha kile alichoagiza. “Mimi sitalihalifu agano langu, Sitalibadili neno lililotoka midomoni mwangu.” (Zaburi 89:34). Tena yeye hana kigeugeu. “Kwa kuwa mimi, Bwana, sina kigeugeu; ndio maana ninyi hamkuangamizwa, enyi wana wa Yakobo.” (Malaki 3:6).
Katika kutafuta kujua nani alibadili siku ya ibada historia inamtaja mtawala wa wakati mmoja wa dola la Kirumi aitwaye Constantine kuwa aliamuru siku ya kwanza ya juma ifanywe kuwa ya mapumziko katika taifa lake. Mtawala huyu ambaye kabla ya kujiunga na Ukristo alikuwa muumini wa dini ya kipagani inayoabudu jua, aliingia madarakani mwaka A.D. 313, na kutoa agizo la kisheria la kuheshimu jumapili tarehe 7, Machi, A.D. 321.
Tangazo hilo linasomeka, Katika Siku ya kuheshimika ya Jua hebu mahakama na watu waishio mjini wapumzike, na hebu karakana zote zipate kufungwa.” — (Codex Justinianus 3.12.3, trans. Philip Schaff, History of the Christian Church, 5th ed. (New York, 1902), 3:380, note 1.)
Hata hivyo Constantine hakuzuia watu kuendelea kupumzika na kuabudu siku ya saba ya juma. Baadaye historia inatujulisha kuwa Kanisa Katoliki ndilo linalojinasibu kufanya uhamisho huo. Kwenye kitabu kiitwacho “The Convert's Catechism of Catholic Doctrine” kilichochapwa 1946 na kuchapwa tena mwaka 1996 na TEACH services inc, na kinachouzwa na Amazon Books kupitia link hiihttps://
Kwenye ukurasa wake wa 50 mwandishi wa kitabu hiki mhashamu Peter Geiermann, amefafanua jambo hilo kwa njia ya maswali na majibu kama ifuatavyo:-
Swali: Siku ya Sabato ni ipi?
Jibu: Jumamosi ndiyo siku ya Sabato.
Swali: Kwa nini tunaiheshimu (tunaitunza) siku ya Jumapili badala ya siku ya Jumamosi?
Jibu: Tunaitunza Jumapili badala ya Jumamosi kwa sababu Kanisa Katoliki katika baraza lake la Laodikia, (AD 336) lilihamisha utakatifu kutoka Jumamosi kwenda Jumapili….
Swali: Kwa nini Kanisa Katoliki liliweka Jumapili badala ya Jumamosi?
Jibu: Kanisa liliiweka Jumapili badala ya Jumamosi kwa sababu Kristo alifufuka kutoka kwa wafu siku ya Jumapili, na Roho Mtakatifu aliwashukia Mitume siku ya Jumapili.
Swali: Ni kwa mamlaka gani Kanisa liliiweka Jumapili kuwa badala ya Jumamosi?
Jibu: Kanisa liliiweka Jumapili kuwa badala ya Jumamosi kutokana na uwingi wa uwezo ule wa kiungu ambao Yesu Kristo aliuweka juu yake!
—Mhashamu. Peter Geiermann, C.SS.R., (1946), p. 50.
Swali linalobaki kwako na kwangu ni kuwa je, ni kweli kuwa badiliko hili linalodaiwa kufanywa na Kanisa Katoliki lina kibali kutoka kwa Mungu au ni jitihada zingine za mwanadamu kubadilisha maagizo ya ibada kama Kaini alivyojaribu kufanya mapema sana katika historia ya mwanadamu? Je mabadiliko haya yanaweza kuathiri chochote juu ya uhusiano wetu na Mungu? Tutaendelea kuyajadili hayo katika makala zetu zijazo. Ukiwa na swali usisite kuuliza maana lengo hapa ni kuelimishana. Mungu akubariki sana.

1 comments:
Write commentsAsante Sana kwa post,ni nzuri.
ReplyEmoticonEmoticon