Tazama, Mwana-kondoo wa Mungu, aichukuaye dhambi ya ulimwengu! Yohana 1:29.
Kwa muda fulani, mvuto wa Mbatizaji kwa taifa ulikuwa mkubwa kuliko ule wa watawala, makuhani au wafalme. Kama angejitangaza kuwa Masihi na kuanzisha uasi dhidi ya Rumi, makuhani na watu wangeenda kwa wingi chini ya bendera yake. Shetani alikuwa amesimama akiwa tayari kumuingizia Yohana Mbatizaji kila namna ya wazo ambalo lilikuwa na mvuto kwa malengo ya wakuu wa kidunia. Lakini akiwa na vithibitisho mbele yake vya uwezo wake, alidumu kukataa rushwa ya ufahari. Usikivu wa wengi ambao ulikuwa umeelekezwa kwake, aliuelekeza kwa Mwingine. Sasa akaona lile wimbi la umaarufu likigeukia mbali naye na kumwelekea Mwokozi. Siku kwa siku umati uliokuwa naye ukapungua….
Wanafunzi wa Yohana walimjia… wakisema, “Rabi, yeye aliyekuwa pamoja nawe ng’ambo ya Yordani, yeye uliyemshuhudia, tazama, huyo anabatiza na watu wote wanamwendea.” Kupitia kwa maneno haya, Shetani alimletea Yohana jaribu. Japo utume wa Yohana ulikuwa karibu kufikia mwisho, bado ilikuwa inawezekana kwake kuzuia kazi ya Kristo. Kama angejihurumia mwenyewe na kuonesha huzuni au kukata tamaa kwa sababu ya nafasi yake kuchukuliwa na mwingine, angepanda mbegu za mfarakano, angetia moyo wivu na kijicho na angezuia maendeleo ya injili kwa kiasi kikubwa sana.
Kwa asili, Yohana alikuwa na kasoro na udhaifu ambavyo ni kawaida kwa binadamu, lakini mguso wa upendo wa Mungu ulikuwa umembadilisha. Alikaa kwenye mazingira ambayo hayakuchafuliwa na ubinafsi na tamaa za makuu na tena mbali sana na mazingira machafu ya kijicho….Ilikuwa ni furaha yake kushuhudia mafanikio ya kazi ya Mwokozi…
Huku akimwangalia Mkombozi kwa imani, Yohana aliinuka hadi kufikia viwango vya kujikana nafsi. Hakutaka kuvutia watu kwake binafsi, bali kuwainua mawazo yao juu na tena juu zaidi, hadi watulie kwa Mwana-kondoo wa Mungu. Yeye mwenyewe alikuwa ni sauti tu, inayolia nyikani. Sasa, kwa furaha alikubali ukimya na hali ya kutokuonekana ili macho ya wote yageuziwe kwake aliye Nuru ya uzima. Wale walio waaminifu kwa wito wao kama wajumbe wa Mungu hawatatafuta heshima kwa ajili yao binafsi. Kupenda nafsi kutamezwa katika kumpenda Kristo.
”Rehema za Bwana ni mpya kila siku asubuhi.”
(Maombolezo 3:22, 23).

EmoticonEmoticon