Inaendelea.......
Lakini hakuna ambaye hana budi kudanganywa na madai ya udanganyifu ya imani ya kuongea na mizimu (Spiritualism). Mungu ameutoa mwanga kwa walimwengu kutosha kuwadhihirishia madanganyo haya. Hata kama ushuhuda mwingine usingekuwako, kuna neno moja ambalo lingetosha Wakristo, ndilo linalosemwa ya kwamba pepo hawaweki tofauti yo yote kati ya wema na uovu, hata ya wanafunzi wanyofu wa Kristo na watumishi wabaya mno wa Shetani. Kwa kuonyesha ya kwamba mtu aliye mwovu kabisa yuko mbinguni, na ya kwamba ameadhimishwa huko, kwa kweli ni kama Shetani huwatangazia walimwengu neno hivi: Haidhuru ukiwa mwovu wa namna gani; haidhuru kama unamwamini Mungu na Biblia au sivyo. Waweza kuishi maisha kama upendavyo; mbinguni makao yako.
Hata mitume, kama wakiigizwa na pepo hawa wa uongo, wanaonyeshwa kana kwamba wanayakanusha maneno waliyoyaandika kwa maongozi ya Roho Mtakatifu walipokuwa hapa duniani. Hukana ya kwamba Biblia ni Neno Takatifu la Mungu, na hivi huuondoa msingi wa tumaini la Wakristo na huizimisha taa inayoangaza njia iendayo mbinguni.
Shetani anawafanya walimwengu waamini ya kwamba Biblia ni kitabu cha hadithi zilizobuniwa tu, au ya kwamba ni kitabu kilichofaa kusomwa na mataifa ya zamani, lakini kwa sasa inafaa kuheshimiwa kidogo tu, ama kufikiriwa kuwa kitu cha zamani kisichotumika siku hizi. Na badala ya Neno la Mungu Shetani huleta maonyesho ya mizimu.
Hapa ndipo njia inayokuwa chini ya utawala wake kabisa; kwa namna hii anaweza kuwafanya watu waamini juu ya mambo yo yote apendavyo.
Kile kitabu kitakachomhukumu Shetani na wafuasi wake hukiweka gizani, kipate kudharauliwa jinsi atakavyo; na humfanya Mwokozi wa wanadamu asiwe na tofauti na mtu ye yote duniani.
Na kama vile askari wa Kirumi waliolinda kaburi la Yesu walivyoeneza habari za uongo kama walivyoambiwa na makuhani na wakuu ili kuikanusha habari ya ufufuo wa Yesu, hivyo ndivyo ambavyo wale wanaoamini juu ya maonyesho ya mizimu wanavyowadanganya watu ya kwamba hakuna mambo ya ajabu wala mwujiza ktk maisha ya Mwokozi wetu. Baada ya kumdharau Yesu hivi, huanza kuwatazamisha watu miujiza yao wenyewe wakisema ya kwamba miujiza hii huishinda ile iliyofanywa na Kristo.
Itaendelea.......

EmoticonEmoticon