“Wala katika wana wa Israeli hakuwako mtu mzuri kuliko yeye”.
1 Samweli 9:2.
Sifa za kitabia za mfalme atarajiwaye zilihitajika zile zenye kufurahisha moyo wa kiburi uliochochea shauku ya kupata mfalme… Mzuri, mrefu, mwenye umbo la madaha, kijana jasiri mwenye nguvu, aonekanaye kuwa alizaliwa ili apate kutawala. Pamoja na mivuto hii tele ya nje, Sauli alikuwa amepungukia sifa bora za kitabia ziundazo hekima ya kweli. Katika ujana wake Sauli alikuwa hajajifunza kutawala tabia yake ya harara na papara; alikuwa hajawahi kupokea neema ihuishayo ya Mungu.._
BWANA hataruhusu Sauli akabidhiwe ofisi yenye majukumu muhimu pasipo kupewa nuru ya Mungu. Sharti apate mwito mpya, hivyo Roho wa BWANA alikuja juu yake. Matokeo yake alibadilishwa kuwa mtu mpya. BWANA alimpatia Sauli roho mpya, mawazo mapya, makusudi na njozi mpya, tofauti na alizokuwa nazo hapo awali. Nuru hii mpya, pamoja na maarifa ya kiroho juu ya Mungu, vilikuwa siri ya ushindi, kuunganisha mapenzi yake na mapenzi ya Yehova . . .
Sauli alikuwa na akili na mvuto uliomwezesha kutawala ufalme, endapo nguvu zake zingesalimishwa katika uongozi wa Mungu, ila vipaji vyenye nguvu ya kumwezesha kutenda mema vyaweza pia kutumiwa na Shetani, iwapo vitasalimishwa mikononi mwake, na hivyo kumwezesha kueneza mvuto mkuu wa uovu. Angeweza kuwa mwenye kulipiza kisasi, kuwa mwenye madhara zaidi na mwenye ari zaidi kutekeleza mipango yake miovu, kuliko wengine, kwa sababu ya vipaji bora vya kiakili na moyo alivyopatiwa na Mungu._
Endapo atatumaini nguvu na akili zake mwenyewe, Sauli ataenenda kwa kukurupuka, na hivyo kutenda makosa mengi ya kutisha. Ila endapo atadumu mnyenyekevu, akitafuta daima kuongozwa na hekima ya Mungu, na kupiga hatua kadri maongozi ya Mungu yafunguapo njia, atamudu kuendesha shughuli za wadhifa wake mkuu kwa mafanikio na heshima. Chini ya mvuto wa neema ya Mungu, kila sifa njema ya kitabia itakuwa ikipata nguvu, wakati kila udhaifu hatua kwa hatua ukipoteza nguvu hadi kutoweka. Hii ndiyo kazi BWANA aahidiyo kuitenda kwa wote waliojisalimisha kwake._
”Rehema za Bwana ni mpya kila siku asubuhi.”
(Maombolezo 3:22, 23).

EmoticonEmoticon