“Nafsi yangu i kati ya simba, Nitastarehe kati yao waliowaka moto.”
Zaburi 57:4.
Ni wa thamani kiasi gani mvuto mwema wa Roho wa Mungu unapoingia kwa mtu aliyepata msongo au aliyekata tamaa, ukitia shime moyo unaozimia, ukitia nguvu walio dhaifu, ukimpatia ujasiri na msaada mtumishi wa Mungu anayejaribiwa. Kwa hakika Mungu wetu ni wa ajabu, anayeshughulika na wakosaji kwa upole na kudhihirisha saburi yake na kudhihirisha huruma yake wakati wa shida, na wakati tunapoelemewa na huzuni.
Kila kushindwa kwa wana wa Mungu kunatokana na kukosa imani. Uvuli unapoizingira nafsi, tunapohitaji nuru na mwongozo, hatuna budi kutazama juu: kuna nuru ng’ambo ya giza. Daudi hakutakiwa kukosa imani kwa Mungu hata mara moja. Alikuwa na sababu ya kumtumaini, alikuwa mtiwa mafuta wa Bwana, na katikati ya hatari alikuwa amelindwa na malaika wa Mungu; alikuwa amejazwa ujasiri ili afanye mambo makubwa ya ajabu; na kama angeondoa mawazo yake katika hali ya kuleta msongo aliyokuwa nayo na kufikiri juu ya uweza wa Mungu na ukuu wake, angeendelea kuwa na amani hata katika uvuli wa mauti…
Katika milima ya Yuda, Daudi alitafuta pa kukimbilia toka kwa Sauli aliyekuwa akimwinda. Alikimbilia kwenye mapango ya Adulamu, mahali ambapo, kwa kutumia kikosi kidogo, angeweza kupadhibiti dhidi ya jeshi kubwa. “Na ndugu zake na watu wote wa mbari ya baba yake waliposikia habari hiyo, wakamwendea huko”…
Katika pango la Adullam familia ilikutanishwa na huruma na upendo. Mwana wa Yese alitunga maneno ya wimbo na sauti na kuimba, “Tazama, jinsi ilivyo vema, na kupendeza, Ndugu wakae pamoja, kwa umoja!”(Zaburi 133:1). Alikuwa ameonja uchungu wa kutoaminiwa na ndugu zake; na mapatano yalikuwa yametokea yaliyoleta furaha kwa moyo wa mkimbizi huyu. Hapa ndipo Daudi alitunga Zaburi 57.
”Rehema za Bwana ni mpya kila siku asubuhi.”
(Maombolezo 3:22, 23).

EmoticonEmoticon