“Basi, Yonathani akamwambia yule kijana aliyemchukulia silaha zake, Haya! Na twende tukawavukie ngomeni hao wasiotahiriwa; yamkini BWANA atatutendea kazi; kwa maana hakuna la kumzuia BWANA asiokoe, kwamba ni kwa wengi au kwamba ni kwa wachache,”
1 Samweli 14:6.
Kwa sababu ya dhambi ya Sauli ya kutoa sadaka ya kuteketezwa kwa jeuri, BWANA hakumpatia heshima ya kuwaangamiza Wafilisti. Yonathani, mtoto wa mfalme, mtu aliyemwogopa Mungu, alitumiwa na Mungu kuleta ushindi kuokoa Israeli. Akisukumwa na wito mtakatifu, alimshauri mbeba silaha wake kwamba wavamie kambi ya adui kwa kushtukiza.
Wao wawili wakaondoka kambini, kwa siri, ili kuepuka wazo lao jema lisije likapata upinzani. Kwa ombi la dhati kwa Mungu wa baba zake, walikubaliana kuhusu ishara ambayo itawapatia mwongozo wa jinsi ya kusonga mbele. Wakiisogelea ngome ya Wafilisti, walionekana machoni pa adui zao, ambao walibeza wakisema, “Tazama, hao Waebrania wanatoka kwenye mashimo walimojificha;” kisha wakawapatia changamoto, “Haya ninyi pandeni hapa juu tulipo, na sisi tutawaonyesha jambo,” ikimaanisha watawapatia kipigo hao Waebrania wawili endapo watathubutu kufika hapo walipo.
Changamoto hiyo ndiyo ishara ambayo Yonathani na mbeba silaha wake waliyokubaliana iwe ushahidi kuwa BWANA atafanikisha mpango wao. Sasa wakiwa hawaonekani machoni pa Wafilisti, wakichagua njia ngumu tena ya siri, mashujaa hao wawili walisonga mbele hadi juu kabisa ya jabali refu mno, la hatari sana, lisilo na ulinzi wa kutosha. Hivyo wakamudu kupenyeza kwa kambi ya adui na kushtukiza walinzi, nao kwa kushtuka na hofu, hawakuonesha upinzani wo wote.
Malaika wa mbinguni walimhifadhi Yonathani na msaidizi wake, malaika walipigana kando yao, nao Wafilisti wakaanguka mbele zao.
Watu hao wawili walidhihirisha kuwa wanatenda kazi chini ya mvuto na maagizo ya Kamanda asiye mwanadamu. Kwa mwonekano wa nje, jitihada zao zilikuwa papara, kinyume kabisa na kanuni zote za kijeshi. Lakini utendaji wa Yonathani haukutokana na papara ya kibinadamu. Hakutegemea mbinu zake za kivita au ubora wa silaha alizokuwa nazo; bali alimtumainia Mungu aliyemwezesha kuleta ushindi kwa niaba ya taifa lake la Israeli.
”Rehema za Bwana ni mpya kila siku asubuhi.”
(Maombolezo 3:22, 23).

EmoticonEmoticon