“Naye mfalme akasema, Kufa utakufa, Ahimeleki, wewe na jamaa yote ya baba yako.”
1 Samweli 22:16.
Watu hawawezi kuyaacha mashauri ya Mungu na bado wakasalia na utulivu na hekima inayowawezesha kutenda kwa haki na busara. Hakuna kuchanganyikiwa kwa hali ya kutisha, na kukatisha tamaa, kama kule kufuata hekima ya kibinadamu, bila kuongozwa na hekima ya Mungu.
Sauli alikuwa akijiandaa kumtega na kumnasa Daudi katika pango la Adullam, na ilipogundulika kwamba Daudi alikuwa amehama mahala pale pa kimbilio, mfalme alikasirika sana. Kuondoka kwa Daudi kulikuwa fumbo kwa Sauli. Alitafsiri kwamba lazima tu kuna msaliti katika kambi yake, ambaye alimjulisha mwana wa Yese juu ya mipango na ukaribu wa Sauli.
Aliwathibitishia washauri wake kwamba njama ilikuwa imepangwa dhidi yake, na kwa ahadi ya zawadi nono na vyeo vya heshima aliwahonga ili wamwambie ni nani miongoni mwao ni rafiki wa Daudi. Doegi Mwedomi akageuka mtoa taarifa. Akisukumwa na tamaa na uchoyo, na kwa kumchukia kuhani, ambaye alikuwa amemkemea kwa sababu ya dhambi zake, Doegi akatoa taarifa juu ya ziara ya Daudi kwa Ahimeleki, akiwasilisha kwa namna ambayo itachochea hasira ya Sauli dhidi ya mtu wa Mungu. Maneno ya ulimi huo wa kifisadi, yaliwasha moto wa kuzimu, yakaamsha hasira ya kutisha katika moyo wa Sauli. Akiwa amepagawishwa na hasira, akatangaza kwamba familia yote ya kuhani itaangamizwa. Na hilo tamko lake la kutisha likatekelezwa. Si Ahimeleki pekee, bali na watu wa nyumba ya baba yake… walichinjwa kwa amri ya mfalme, kwa mkono wa uuaji wa Doegi.
Hiki ndicho Sauli alifanya chini ya utawala wa Shetani. Mungu aliposema kwamba uovu wa Waamaleki ulikuwa umejaa, na kumwagiza kuwaangamiza kabisa, alijiona kuwa na huruma mno kiasi cha kutotekeleza hukumu ya Mungu, na kukiachilia kile ambacho kilitakiwa kuangamizwa; lakini sasa, bila amri ya Mungu, chini ya udhibiti wa Shetani, aliwachinja makuhani wa Bwana na kuleta uangamivu kwa wakazi wa Nob. Ndivyo ulivyo upotovu wa moyo wa mwanadamu ambao umeyakataa maelekezo ya Mungu.
”Rehema za Bwana ni mpya kila siku asubuhi.”
(Maombolezo 3:22, 23).

EmoticonEmoticon