“Basi, mtoto Samweli akamtumikia Bwana mbele ya Eli.”
1 Samweli 3:1.
Licha ya udogo wake wakati alipoletwa kuhudumu hekaluni, hata kwa umri ule Samweli alikuwa na huduma za hekaluni alizomudu kuzitenda kwa BWANA, kulingana na uwezo wake. Mwanzoni huduma hizo zilikuwa ni zile za hadhi ya chini, zisizovutia; lakini alizitenda kwa weledi mkuu, kwa moyo mweupe wa kujituma.
Iwapo watoto wangalifundishwa kuheshimu shughuli ndogo ndogo za kila siku kama kazi waliyopewa na BWANA, kwamba ni shule ambayo kupitia kwayo wanajifunza kutoa huduma bora ya uaminifu, kazi hizo wangaliziona za kupendeza na za heshima kuu. Kutenda kila jukumu kama kwamba watenda kwa BWANA, huleta fahari kwa kazi duni na kuwafungamanisha watendakazi duniani na viumbe watakatifu wa mbinguni ambao hutenda mapenzi ya Mungu mbinguni.
Maisha ya Samweli tangu utoto yamekuwa maisha ya unyenyekevu na kumcha Mungu. Aliwekwa chini ya uangalizi wa Eli katika ujana wake, na tabia yake njema ilimvutia kuhani huyo mzee. Alikuwa mkarimu, chapakazi, mtiifu, na mwenye adabu. Mwenendo wa kijana huyu ulikuwa bora na wa kuigwa, kinyume kabisa na vile walivyokuwa wana wa Eli, hivyo kupata faraja, amani, na baraka atendapo kazi na kijana huyo. Inashangaza kwamba Eli, mwamuzi mkuu wa Israeli, alikuwa anamheshimu kijana huyo mdogo sana, na kuwa na matumaini makubwa kwake. Samweli alikuwa mtiifu na chapakazi, na hakika hakuna baba aliyewahi kuonesha upendo mkuu kwa mwanawe kama vile Eli alivyoonesha kwa kijana Samweli. Kadri uzee ulivyomsonga Eli, alizidi kusononeshwa na tabia mbaya ya wanawe, hivyo akawa anapata farijiko na msaada kutoka kwa Samweli.
Inapendeza jinsi gani kuona kijana na mzee wanasaidiana na kutegemeana; kijana akihitaji ushauri na hekima za mzee, na mzee akitaraji msaada na huruma kutoka kwa kijana. Hivyo ndivyo ipaswavyo kuwa. Mungu angalipenda vijana wawe na sifa za kitabia zenye mvuto kwa wazee, kwamba waweze kujumuika pamoja katika pendo la kweli na wale ambao maisha yao yako mbioni kukoma.
”Rehema za Bwana ni mpya kila siku asubuhi.”
(Maombolezo 3:22, 23).

EmoticonEmoticon