TAMBUA MTEGO WA SHETANI JUU YA MPANGO WA WOKOVU



Msidhani ya kuwa nalikuja kuitangua torati au manabii; la, sikuja kuitangua, bali kutimiliza. Kwa maana, amini, nawaambia, Mpaka mbingu na nchi zitakapoondoka, yodi moja wala nukta moja ya torati haitaondoka, hata yote yatimie. 
Basi mtu yoyote atakayevunja amri moja katika hizi zilizo ndogo, na kuwafundisha watu hivyo, ataitwa mdogo kabisa katika ufalme wa Mbinguni; bali mtu atakayezitenda na kuwafundisha, huyo ataitwa mkubwa katika ufalme wa Mbinguni.
Mathayo 5:17 - 19.

Shetani hawezi kuzuia mpango wa wokovu. Yesu alisulubishwa na akafufuka siku ya tatu. Lakini Shetani aliwaambia malaika zake kuwa angefanya kusulubishwa na kufufuka kwa Yesu kuwa faida yake. Alikusudia kwamba wale wanaodai kumwamini Yesu, waamini kuwa amri zinazohusiana na kafara na dhabihu za kiyahudi zilikomeshwa na kifo cha Yesu, na angeweza kuwapeleka mbali awafanye waamini kuwa amri kumi zilisulibishwa pamoja na Kristo.

Niliona kuwa wengi walikubali kabisa mpango huu wa Shetani.
Mbingu yote ilichukizwa walipoona Amri Takatifu za Mungu zikikanyagwa chini ya miguu. Yesu pamoja na jeshi lote la mbinguni walifahamu asili ya amri za Mungu; walijua kuwa asingezibadili au kuzitangua. Hali ya mwanadamu isiyo na matumaini baada ya kuanguka kwake ilisababisha huzuni kuu mbinguni, na Yesu akaguswa kujitoa kafara kwa ajili ya mwanadamu aliye asi sheria takatifu ya Mungu. Lakini kama sheria hiyo ingeweza kutanguka, mwanadamu angeweza kukombolewa bila kifo cha Yesu. Kwa hiyo kifo chake hakikuondoa amri za Baba yake, bali kilitukuza na kuadhimisha na kutaka kutii kwa amri zake zote takatifu.

Kama kanisa lingeendelea kuwa safi na imara Shetani asingeweza kuwadanganya na kuwaongoza wazikanyage amri za Mungu. Katika mpango huu wa ufedhuri, Shetani hupingana waziwazi na msingi wa mamlaka ya Mungu mbinguni na duniani.
Uasi wake ulimfanya afukuzwe mbinguni. Baada ya kuasi kwake ili aweze kujiponya alitamani Mungu aibadili amri yake, lakini aliambiwa mbele ya Jeshi lote la mbinguni kuwa amri za Mungu hazibadiliki. Shetani anajua kwamba kama akiweza kuwafanya wengine waivunje amri ya Mungu, tayari amewapata katika kazi yake; kwa maana kila avunjaye amri ya Mungu hana budi kufa.

Bado Shetani alidhamiria kusonga mbele. Aliwaambia malaika zake kuwa wengine watakuwa na wivu sana wa amri za Mungu na kuwa hawataweza kunaswa katika mtego huu. Amri kumi zilikuwa wazi kabisa kiasi kwamba wengi wangeamini kuwa ziliendelea kuwepo na kwa hiyo lazima ajitahidi kuharibu amri moja tu kati ya zote. Kisha akawaongoza mawakala wake kuthubutu kubadili amri ya nne au Sabato, hivyo ndivyo alivyoibadili amri moja kati ya kumi, inayomwonyesha Mungu wa kweli Muumba wa mbingu na nchi. Shetani aliwaonyesha Ufufuo mtukufu wa Yesu na kuwaambia kwamba kwa kufufuka kwake siku ya Kwanza ya juma, alibadili Sabato toka siku ya saba ya juma kwenda siku ya Kwanza ya juma.

Hivyo ndivyo Shetani alivyotumia Ufufuo wa Yesu ili kutimiza makusudi yake. Yeye na malaika zake walifurahia kwamba uongo waliobuni ulipokelewa vizuri na wale wanaojidai kuwa marafiki wa Kristo kile ambacho mmoja anakiangalia kama chukizo la kidini mwingine alikipokea. Hivyo ndivyo uongo tofauti ulivyopokelewa na kutetewa kwa bidii. Mapenzi ya Mungu, yaliyofunuliwa wazi katika Neno lake, yalifunikwa na uongo na mapokeo, vilivyokuwa vikifundishwa kama amri za Mungu. Ingawa udanganyifu huu mkuu utaruhusiwa uendelee mpaka Yesu atakapoonekana mara ya pili, lakini katika vipindi hivi vyote vya uongo na udanganyifu, Mungu alikuwa na mashahidi waliokuwa wamesalia. Katika giza na mateso ya kanisa daima kulikuwepo na waaminifu wa kweli waliotunza amri zote za Mungu.
(Maandiko ya Awali, uk. 217, 218.)

”Rehema za Bwana ni mpya kila siku asubuhi.”
(Maombolezo 3:22, 23).

Image may contain: cloud, sky and outdoor
Previous
Next Post »
Powered by Blogger.