“TUFANANE NA MATAIFA MENGINE”



“Sivyo hivyo; lakini tunataka kuwa na mfalme juu yetu; ili sisi nasi tufanane na mataifa yote.”
1 Samweli 8:19, 20.

Waebrania walimwendea Samweli kutaka wapate mfalme, kama mataifa yanayowazunguka.Kwa kutaka mfalme mtawala badala ya serikali ya hekima na upole ya Mungu, iongozwayo na manabii wake; walionesha upungufu mkuu wa imani kwa Mungu, na tumaini kwa maongozi yake kwamba aweza kuinua mtawala juu yao apate kuwaongoza. Wana wa Israeli wakiwa ni taifa teule la Mungu, muundo wa serikali yao ulikuwa tofauti kabisa na serikali za mataifa yanayowazunguka. Mungu amewapatia kanuni na sheria zake, na amekuwa akiwachagulia viongozi, na watu walipaswa kuwatii viongozi hao katika BWANA. Wakati wa dhiki na zahama kuu, walipaswa kumwuliza Mungu.

Tamko lao kutaka mfalme ulikuwa ukataaji dhahiri kwamba Mungu, aliye kiongozi wao maalumu, hawamtaki tena awe kiongozi juu yao. Alijua kwamba mfalme hatakuwa kiongozi bora kwa watu wa Mungu. Watakapokuwa na mfalme, ambaye ana kiburi, asiyempenda Mungu, atawatenga mbali na Mungu, akiwaongoza wamwasi Mungu. BWANA alijua kuwa hakuna mtu awezaye kupata cheo cha ufalme, apokee heshima zimstahizo mfalme, asijaribiwe kujitukuza nafsi, huku watu wakitenda waonayo mema machoni pao, kumbe wanatenda dhambi dhidi ya Mungu.

Mungu alikuwa amelitenga taifa la Israeli mbali na mataifa mengine, liwe hazina yake ya pekee. Ila walipuuzia heshima hii kuu waliyopewa, wakawa wanataka kuiga mwenendo wa mataifa! Na hata leo shauku ya kuiga mienendo na desturi za mataifa ni jambo linalosumbua Wakristo wa leo. Kadiri wanavyojitenga mbali na Mungu wanajawa shauku ya kutaka mali na heshima ya dunia. Wakristo daima wanatafuta kuiga mienendo ya wale wanaoabudu mungu wa dunia hii. Wengi hudai kuwa kwa kujifungamanisha pamoja na watu wa dunia na kufuatisha desturi zao lengo lao ni kuwavuta waachane na mwenendo wao mwovu. Ieleweke kuwa wote wafanyao hivyo hujitenga mbali na yeye aliye chimbuko la uweza. Kwa kutafuta kuwa rafiki wa ulimwengu, wanaamua kuwa adui za Mungu.

”Rehema za Bwana ni mpya kila siku asubuhi.”
(Maombolezo 3:22, 23).

Image may contain: text
Previous
Next Post »
Powered by Blogger.